Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, taasisi za kidini nchini Tanzania, Kenya na Uganda zimeonesha dhamira ya dhati ya kuhuisha mafunzo na ujumbe wa Karbala kupitia programu mbalimbali za kidini, kielimu na kiutamaduni zitakazofanyika katika kipindi chote cha Muharram.
Katika siku za hivi karibuni, taasisi hizo zimekuwa zikisambaza mabango, matangazo na ujumbe maalumu kupitia mitandao ya kijamii, huku zikiwahamasisha waumini kuhudhuria Majlisi za maombolezo ya Imam Hussein (as), ambazo hutoa fursa ya kujifunza kuhusu misingi ya haki, uadilifu, kujitolea na kusimama dhidi ya dhulma.
Taarifa zinaonesha kuwa nchi za Afrika Mashariki ni miongoni mwa maeneo ambayo kila mwaka hushuhudia ushiriki mkubwa wa waumini katika shughuli za Muharram, huku misikiti, husainiya na vituo mbalimbali vya Kiislamu vikijiandaa kupokea mamia ya washiriki katika vikao hivyo vya kiroho.
Miongoni mwa taasisi zilizotangaza ratiba na maandalizi ya Majlisi za Muharram ni Taasisi ya Imam Sadiq (as), Tanzania Ithna-Ashari Community (TIC), Taasisi ya Ummul Baniin, Bilaal Muslim Mission pamoja na taasisi nyingine za kidini zinazofanya kazi ya kueneza mafundisho ya Ahlulbayt (as) katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Waandaaji wa shughuli hizo wamewataka waumini kutumia fursa ya mwezi wa Muharram kujifunza kwa kina historia ya Karbala, kuimarisha maadili ya Kiislamu na kuhuisha ujumbe wa Imam Hussein (as), ambao umeendelea kuwa alama ya kusimamia haki, heshima na uadilifu katika nyakati zote.
Maadhimisho ya Muharram yanatarajiwa kufanyika katika miji mbalimbali ya Afrika Mashariki, huku yakihusisha mihadhara, vikao vya maombolezo, usomaji wa Qur'ani Tukufu, pamoja na shughuli nyingine za kidini zinazolenga kuenzi kumbukumbu ya mashahidi wa Karbala.
Inafaa kujatwa kwamba; baadhi ya Taasisi hizo zilianza ratiba zao za Majlisi siku ya jana usiku huku nyengine zikianza rasmi leo hii.












Maoni yako